Ijumaa, 8 Novemba 2013

PROF.MAGHEMBE AMEKUMBUSHWA KUWAPATIA WANANCHI MAJI HASA HUKO VIJIJINI


maghembe_300_277
MBUNGE wa Viti Maalum, Leticia Nyerere (Chadema), amemtaka Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kwenda Kwimba mkoani Mwanza na kuishi huko kwa siku tano bila kuoga, ili ajue adha ya maji inayowakabili wakazi wa Mji wa Ngudu.
Leticia alitoa kauli hiyo, wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni leo, ambapo alitaka kujua ni lini Mji wa Ngudu wilayani Kwimba utapata maji.
Akijibu swali hilo, Profesa Maghembe alisema Septemba mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alitembelea mji huo na kuagiza upatiwe maji katika muda wa miezi sita. Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, utekelezaji wa mradi huo umeanza na unatarajia utakamilika ndani ya miezi sita kama ilivyoahidiwa na Rais Kikwete.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mahmoud Mgimwa (CCM), alihoji Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo sugu la maji katika Halmashauri ya Mji mdogo wa Mafinga, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya maji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa, alisema Mji mdogo wa Mafinga una wakazi 51,902, ambapo asilimia 63 ndiyo wanapata maji safi na salama.
Alisema mahitaji ya maji kwa wakazi wa Mafinga ni meta za ujazo 3,633 kwa siku, sawa na lita milioni 3.6 kwa siku wakati maji yanayozalishwa kutoka vyanzo vilivyopo, ni meta za ujazo 2,877 kwa siku sawa na lita 2.87 au asilimia 97.2 ya mahitaji.
Kutokana na hali hiyo, upungufu wa maji kwa wakazi wa eneo hilo alisema ni meta za ujao 756 kwa siku sawa na lita 756,000 kwa siku ikiwa ni sawa na asilimia 20.
Alisema ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mafinga, Serikali kupitia Wizara ya Maji imefanya usanifu wa mradi mkubwa ambao utahusisha ujenzi wa bwawa lenye ukubwa wa mita za ujao milioni 2.8 ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
Alisema upanuzi wa mradi wa maji katika Mji wa Mafinga unakadiriwa kugharimu jumla ya Sh milioni 60.7.
Aidha, Mamlaka ya Maji Mafinga kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ipo katika mpango wa kukopa kiasi cha Sh milioni 319 kutoka taasisi za kifedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kutoka Mji wa Mafinga na kufanya upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya maji iliyopo.
Alisema miradi hiyo ikikamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji na hivyo kuondolea adha wananchi ya kutafuta maji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni