Ijumaa, 15 Novemba 2013

JUMUIYA YA MADOLA IMEANZA MKUTANO HUKO NCHINI SRI LANKA

Maandamano kupinga mkutano huo kufanyika Sri Lanka


Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa jumuiaya ya madola, umeanza nchini Sri Lanka, lakini mkutano huo umegubikwa na mjadala mkali ikiwa ilikuwa sawa kuandaa mkutano huo nchini humo.
Canada, India na Mauritius wamesusia mkutano huo wakilalamika kuwa serikali ya Sri Lanka ilikataa kuchunguza madai ya ukikuwaji wa haki za binadamu wakati serikali ilipokuwa inapambana na waasi wa Tamil Tigers na kushinda mwaka 2009.

Waziri mkuu wa Uingeza anahudhuria mkutano huo, lakini atafanya ziara nyingine hadi maeneo la kaskazini mwa Sri Lanka kukutana na viongozi wa Tamil ili kuelezea wasi wasi wake.Rais Mahinda Rajapaksa amewashukuru watu waliohudhuria mkutano huo na kuinga mkono nchi yake.
Warsha hiyo imefunguliwa huku mwana mfalme Prince Charles,akimwakilisha mama yake Malkia Elizabeth, kama mkuu wa Jumuiya ya Madola .
Mkutano huu umeanza kuhusu mkutano mwingine uliokuwa unaangazia haki za binadamu mjini Colombo ukifungwa na maafisa wakuu nchini humo.
Mkutano huo hata hivyo ulitarajiwa kufungwa. Mnamo Jumatano na Alhamisi mkutano huo ulivamiwa na makundi yanayounga Serikali mkono, kukiwemo na watawa wa Kibudha na hali hiyo ilitokea baada ya muda Polisi kuamuru kuwa mkutano huo ufungwe.
Tayari maafisa wa usalama Kaskazini mwa Siri Lanka walikuwa wamezuia mabasi yaliyokuwa yamewabeba watu wa kabila la Watamil kuelekea Colombo kwa mkutano huo wa Haki za Kibinadamu.
Mashirika ya kiraia kwa wakati huu yanajitahidi kadiri ya uwezo wao kujaribu kupata habari kuwahusu maelfu ya watu waliotoweka; wengine wao kuanzia mwaka 1990.
Hadi kufikia sasa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, pamoja na mwana Mfalme wa Uingereza, Prince Charles, wamefika nchini Sri Lank kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Madola. Prince Charles atafungua rasmi mkutano huo akimwakilisha mamake, Malkia Elizabeth wa Uingereza.
Siku chache zilizopita Bwana Cameron na viongozi kadhaa wa Sri Lanka wamekuwa wakijibizana vikali kufuatia tangazo la Bwana Cameron kuwa atazua mjadala wa hali mbovu ya haki za kibinadamu nchini Sri Lanka. Lakini viongozi wa Sri Lanka wamesema kuwa hawatamruhusu kuzusha mjadala huo ambao Serikali hiyo, mwenyeji wa mkutano huo inaona kama ni madharau.
Bwana Cameron ametetea ziara yake ya Sri Lanka, licha ya makundi kadhaa kumshauri aususie mkutano huo kwa sababu za ukiukaji wa haki za kibinadamu wa taifa hilo. Kwa upande wake Cameron amesema ukiukaji huo ambapo wanajeshi waliwatendea unyama waasi wa Tamil Tiger ni swala ambalo lazima alizungumzie.
Waziri Mkuu huyo wa Uingereza alisisitiza kuwa ni heri ajitokeze na kuangazia swala hilo akiwa mkutanoni ngambo badala ya kukaa nyumbani.
Mkereketwa wa Haki za Kibinadamu wa Sri Lanka, Brito Fernando, amesema kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kupida darubini kwa yote yanayoendelea nchini Sri Lanka.

MTU MMOJA AMBAE NI KASISI AMETEKWA NYARA NCHINI CAMEROON



Kasisi mmoja mfaransa ametekwa nyara Kaskazini mwa Cameroon karibu na mpaka wa Nigeria. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa.
Kasisi huyo, Georges Vandenbeusch alitekwa nyara mapema asubuhi mnamo siku ya Alhamisi, umbali wa kilomita 30 kutoka mpakani.

Kundi la wapiganaji wa Boko Haram, wanajulikana kuendeshea harakati zao katika eneo hilo.Takriban watu 15 waliokuwa wamejihami, walivamia makao ya Nguetchewe ambako kasisi huyo alikuwa akifanya kazi , kulingana na askofu mkuu.
Askofu mkuu ambaye kasisi huyo alikuwa chini yake, alisema kua kijisanduku cha kasisi huyo kilipatikana barabarani
Baadhi ya waliofanya kazi na kasisi huyo walisema kuwa watekaji nyara walifika kwa miguu kumteka nyara kasisi na kuwa walikuwa wanaongea kiingereza.
Msemaji wa serikali ya Cameroon, Issa Tchiroma Bakary,alisema kuwa maafisa wanahofia kwamba kasisi huyo tayari ameondolewa nchini.
Kwa mujibu wa maafisa wakuu, huenda wapiganaji wa Boko Haram ndio waliomteka kasisi huyo.
Rais Francois Hollande, amesema kuwa wanafanya kila hali kuhakikisha kuwa kasisi huyo ataachiliwa.
Akizungumza mjini Monaco, aliwasihi raia wa Ufansa kutohatarisha maisha yao.
Mapema mwaka huu, jamaa saba wa familia moja , wanne kati yao watoto, walitekwa nyara na wapiganaji wa kiisilamu na kuzuiliwa kwa miezi miwili.

WATU WATANO WANASHIKILIWA WAKITUHUMIWA KATIKA SAKATA LA MENO YA TEMBO


Meno ya tembo yaliyokamatwa


Jeshi la polisi  nchini Tanzania wamesema shehena ya meno ya tembo yaliyokamatwa katika bandari ya Zanzibar ni sawa na tembo mia tatu na watano, yakiwa na thamani ya karibu shilingini bilioni nane, sawa na karibu dola milioni tano za Kimarekani.
Watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na meno hayo, huku maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, na mmoja wa Mamlaka ya Bandari pia wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Meno hayo ya tembo yalikuwa yamefichwa kwenye kontena la urefu wa mita 40, tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.Kwa mujibu wa afisa habari mkuu wa jeshi la polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, watuhumiwa wa kesi hii watafikishwa katika mahakama jijini Dar es Salaam.
Serikali ya Tanzania iko katika kampeni kamambe ya kupambana na ujangili ili kunusuru wanyama pori ambao wako hatari kutoweka kutoka na kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na vipusa vya faru.
Iliripotiwa kuwa wastani wa tembo 30 huuawa kila siku nchini Tanzania, hali iliyoilazimisha serikali kukabiliana na mtandao wa ujangili, ambao unatuhumiwa kuunganisha watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wawindaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi.
Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.

BADO HALI NI TETE NCHINI UFILIPINO MARA BAADA YA KIMBUNGA HAYAN

Wakaazi wengi bado wangali kupata msaada


Waziri wa mambo ya ndani wa Ufilipino, amesema kuwa idadi kamili ya watu waliojeruhiwa kutokana na Kimbunga Haiyan, wiki jana, imefika watu elfu tatu na miatano.
Bwana Mar Roxas amekiri kuwa idadi hiyo hata hivyo huenda ni kubwa zaidi ya hiyo.

Ameongeza  kuwa serikali italazimika sasa kuanz akufanya mipango ya ujenzi mpya na wa kudumu.Ingawa idadi rasmi ya waliofariki bado haijulikani na maafisa katika moja ya majimbo yaliyoathirika zaidi kuliko yote, wanasema kuwa watu elfu nne wamefariki jimboni humo pekee.
Serikali inakadiria uhariobifu uliotolkea kuwa wenye thamani ya dola bilioni 15.
Asilimia tisini ya nyumba zimeharibika na maefi ya shule haziwezi tena kutumika.
Watoto hawaedni tena shule hadi mwezi Januari.
Wakati huohuo, wafanyakazi wa kutoa misaada nchini wametaja hali iliyoko nchini humo kama ya kusikitisha, wiki moja tu baada ya kimbunga haiyan kupiga maeneo ya kati ya nchi hiyo. Maelfu ya raia wa nchi hiyo bado wanahitaji misaada ya dharura.
Msemaji wa shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka, la Medcins sans Frontiers, Henry Gray, amesema masuala mengi ya mipango yanaathiri shughuli ya kusambaza misaada.

Katibu mkuu wa muungano wa nchi wanachama wa muungano wa asia na pacific ASEAN Lee lair-un min amesema misaada zaidi itatolewa na kuwa mataifa yote duniani yanaweza kufanya mengi zaidi kusaidia.

WASANII WA MUZIKI WAISIFU "MBEYA CITY FC"

 
Mbeya City 
Wale wakali wa masauti vocal za uhakika na melody za maana Afro Magic Iliyochini ya label ya Hit maker wa Surprise,Nani kama mama na come come yaani namzungumzia Lucky junior the tiger producer mwenye umri mdogo kuliko wote tanzania ambaye pia ni mmiliki wa studio za Magic Records  na Smart Creation Media

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/mbeya-city-sept23-2013.jpg
Jana katika HOT CHEMBA na etco the best kiongozi wa kundi hilo ambaye pia ni mwenyekiti wa lebo ya Afro Magic ambaye pia ni mkali wa ngoma ya Igolo pamoja  na Wale alifunguka na kusema kuwa wao kama Afro Magic wanafurahishwa na timu ya Mbeya City pia alisema kuwa kwa uwezo wa timu hiyo inastaili kusifiwa na kupewa hongera sana pia alisisitiza kuwa lazima ukijari na kukiheshimu kifanyao mazuri 
Samaiko alisisitiza kuwa Mbeya City ni timu iliyojipanga na inaweza mpira na ndiyo maana amna mechi waliyoshindwa zaidi ya droo jamani mbeya city ni ya ukweli na inajiweza Pia samaiko alisisitiza kuwa timu hii imejipanga sana akatoa mfano kuwa kwa wale waliokuwa wametazama mechi ya azam na mbeya city akasema Mwagane Yeya  alifanya kufuru tazama video hii ili ujue Ama kweli Mbeya City kama Barcelona tazama mwagane alichowafanya Azam

 

Jumatano, 13 Novemba 2013

MSWAADA WA KUHUSU NDOA HUENDA UKAPATA SULUHISHO NCHINI KENYA

Wanandoa wataondoka na walichochuma katika ndoa


Bunge nchini Kenya limepitisha mswada wa ugavi wa mali kati ya wanandoa baada ya kutalikiana. Mswada huo unaeleza kwamba mwanamume au mwanamke atapata sehemu ya mali aliyochuma wakati wa ndoa iwapo wataamua kuachana.
Katiba ya sasa inaeleza wazi kuhusu haki sawa kati ya wanandoa kabla, wakati na hata baada ya kuvunjika ndoa. Inaeleza kwamba mali inayomilikiwa wakati wa ndoa itagawanywa nusu kwa nusu baina ya mume na mke iwapo wataachana. Wabunge wanawake nchini wanataka muongozo usalie kama ulivyo.

.
Idadi kubwa ya wabunge wanaume walipiga kura kwa uwingi wa kura 87 dhidi ya wabunge wanawake 28 kuibadili sheria hiyo. Mabadiliko mengine katika mswada huo ni kwamba, mali iliyo katika jina la mwanandoa mmoja sio mali ya wanandoa wote wawili. Mjadala mkali ulizuka bungeni wakati wa ilipopendekezwa kukarabati kipengee kinachoeleza aina ya mali katika ndoa.
Pendekezo lililotolewa ni kwamba mali ya ndoa ni chochote kinachoweza kubebeka na kisichoweza kubebeka kinachomilikiwa na wanandoa wote au kilichonunuliwa wakati wa ndoa.
Sehemu kubwa ya wabunge wanawake waliwashutumu wenzao wanaume kwa kupitisha mswada huo ambao wameutaja kwenda kinyume na katiba. Wameeleza kwamba katika tamaduni za Kiafrika, kwa kawaida mali yote huwa chini ya jina la mume na hivyo iwapo mswada huo utakuwa sheria, utakuwa ni kama kutowatendea wanawake haki. Mswada huo unaonekana kama pigo kwa wamama wasiokuwa na ajira, lakini wanaosaidia katika kuiendeleza familia katika njia nyengine kando na za kifedha. Wabunge wanawake wanaamini kazi za nyumbani, kuitunza na kuiangalia familia, ukulima miongoni mwa majukumu mengine ya wanawake nyumbani ni sehemu ya mchango usio wa kifedha unaopaswa kujumuishwa katika sheria hiyo.
Wakati ikisubiriwa kuona iwapo rais Uhuru Kenyatta atatia saini na kuudhinisha mswada huo kuwa sheria, swali sasa ni je wakati umewadia kwa mataifa ya Afrika kuidhinisha mikataba ya kugawana mali kabla ya ndoa kama ilivyo kwa mataifa ya magharibi?

UN KUONGEZA KIKOSI CHA MAJESHI AMISOM


Kikosi cha Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM)
Kikosi cha Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM)
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeagiza  nyongeza ya wanajeshi elfu nne zaidi kusaidia kikosi cha Umoja wa Afrika kinachopambana na wanamgambo wa Somalia.

 Baraza hilo pia liliidhinisha Umoja wa Mataifa kutoa msaada wa chakula , maji na vifaa vingine kwa jeshi la kitaifa la Somalia,wakati linapofanya operesheni za pamoja na kikosi cha Umoja wa Afrika nchini humo kinachojulikana kama AMISOM.

Uingereza ilidhamini azmio hilo kupitia balozi wake katika Umoja wa Mataifa Mark Lyall Grant. Balozi huyo alisema kikosi cha AMISOM kimefanya juhudi kubwa kudhoofisha nguvu za  kundi la wanamgambo wa al- Shabab.

MCHEZAJI SOKA AMETEMWA KATIKA KIKOSI KISA MORSI


Ahmed Abdul Zaher amejitetea akisema hakunuia kuzua hisia za kisiasa
Mchezaji soka mmoja katika moja ya vilabu maarufu nchini Misri ametupwa nje ya mechi za klabu hiyo baada ya kuonekana kumuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi.
Klabu ya Al Ahly, imesema kuwa Ahmed Abdul Zaher , hatashiriki mchuano wa FIFA wa klabu bingwa duniani baada ya kupiga saluti ya vidole vinne mnamo siku ya Jumapili.

Ishara hio imekuwa ikitumika kama ishara ya kumuunga mkono bwana Morsi.Mchezaji huyo alikuwa anasherehekea bao lake la mchuano wa mabingwa wa Afrika ambapo Al Ahly ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Orlando Pirates wa Afrika Kusini.
Ishara hiyo pia ilitokana na maandamano ya wafuasi wa Morsi waliotawanywa na maafisa wa usalama mnamo mwezi Agosti baada ya kukesha katika eneo walilosema alikuwa amezuiliwa Morsi.
Rais Morsi alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, na sasa anakabiliwa na kesi ya kuchochea mauaji ya waandamanaji wakati wa ghasia zilizotokea mjini Cairo mwaka jana.
Yeye mwenyewe aling'olewa kutoka uongozini mwezi Julai.
Abdul Zaher alisherehekea kwa ishara ya vidole vinne baada ya kuingiza bao la Al Ahly la pili ambapo waliibuka washindi dhidi ya Orlando Pirates.
"ndio nilitoa ishara hiyo ya Rabaa," alinukuliwa akisema kwenye mtandao wa FilGoal.
"lakini sikunuia kuzua hisia za kisiasa kwa mtu yeyote, nilichonuia ni kumkumbuka mtu yeyote aliyefariki, awe raia wa kawaida au hata polisi.''
Mnamo siku ya Jumatatu maafisa wa klabu ya Al Ahly, walisema kuwa Ahmed Abdul Zaher hatashirikishwa kwenye mechi itakayochezwa nchini Morocco.

ISRAEL HUENDA IKASITISHA UJENZI NCHINI PALESTINA

Ujenzi wa makazi ya walowezi wa Israel Palestina


Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amemuagiza waziri wa Nyumba nchini humo kuangalia upya mpango wa ujenzi wa zaidi ya nyumba 20,000 katika eneo la Ukingo wa magharibi mwa mto Jordan.
Netanyahu amesema mpango huo uliotangazwa jumanne wiki hii na waziri wa Nyumba Uri Ariel unaweza kuleta mvutano usio wa lazima na jumuiya ya kimataifa kufuatia Palestina kudai kuwa watakata rufaa umoja wa mataifa Israeli.

Hata hivyo Waziri wa Nyumba wa Israel Ariel amekubaliana na ombi la Waziri wake mkuu kuhusiana na utata wa mpango huo na uwezekano wa kuweza kuahirisha mpango huo.Amesema mpango huo hauna mchango wowote kwa Wayahudi na unakuja wakati ambao kunafanyaika jitihada za kipindi ambacho kuna jitihada za kimataifa katika kufikia muafaka mzuri na Iran kutokana na mzozo wa muda mrefu baina yao.Netanyau pia akizungumzia jambo hilo amerejea mazungumzo ambayo yalishindwa kufikia muafaka yaliyofanyika Geneva kuhusiana na kuhusiana na mpango wa Tehran.
Palestina inataka kusitishwa kwa ujenzi huo ambapo hivi karibuni Rais wa palestina Mahmoud Abbas alitahadhalisha juu ya mpango na kudai kuwa unaweza kuathiri muafaka wa mazungumzo yanayoendelea
Palestina inataka taifa lake kujumuisha eneo lake lote pamoja na lile lililochukuliwa na Israel mwaka 1967 ambapo kwa sasa zaidiya Wayahudi 500,000 wanaishi katika makazi zaidi ya 200 katika eneo hilo la ukingo wa magharibi wa mto Jordan mashariki mwa Jerusalem
Hata hivyo pamoja na kumtaka waziri wake wa Nyumba kufikiria upya juu ya ujenzi wa makazi hayo Netanyahu amekataa kurejeshwa Palestina maeneo yanayodaiwa kuwa yalichukuliwa kabla ya mwaka 1967 na kwamba hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya mipaka.

IDADI YA VIFO NCHINI UFILIPINO IMEAPUNGUA

Waathirika wa kimbunga Ufilipino


Serikali ya Ufilipino imesema zaidi ya watu elfu moja mia nane wamethibitika kufa kufuatia kimbunga Haiyan.
Rais Benigno Aquino amesema anafikiri idadi ya awali iliyotajwa kuwa watu elfu kumi wameuawa katika kimbunga Haiyan ilikuwa kubwa mno, akisema idadi halisi huenda ikawa watu elfu mbili na mia tano.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na maafisa wa usimamizi wa majanga, zinaonyesha kuwa zaidi ya nyumba elfu themanini na watu wapatao laki sita hawana makaazi.Lakini kauli ya Rais Aquino inapingana na maelezo ya maafisa kadha ambao wansema idadi iliyotolewa mwanzoni ya watu elfu kumi kufa kutokana na kimbunga Haiyan ni sahihi.
Wakati huo huo, watu wanane wameuawa nchini Ufilipino wakati watu walionusurika katika kimbunga Haiyan walipojaribu kuvamia ghala la kuhifadhia mchele ili kujipatia chakula.
Watu hao wamekufa wakati ukuta wa jengo ulipoporomoka katika mji wa Tacloban ulioharibiwa vibaya kutokana na kimbunga Haiyan.
Mbunge mmoja kutoka eneo hilo, Martin Romualdez, ameonya kuwa watu wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji na dawa.
Pia amesema kuvunjwa kwa sheria na kanuni nyingine za usalama kunakwamisha usambazaji wa misaada na kwamba hali ya dharura inatakiwa kuchukuliwa na serikali kuu.
Bwana Romualdez amesema mji wa Tacloban umeharibiwa vibaya, mithili ya kupigwa na bomu la nyuklia na kwamba utalazimika kujengwa upya kabisa

BURIANI MTETEZI WA HAKI KWA RAIA DR.MVUNGI



DkMvungi_484_280
Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.
Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.
“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.
Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.
Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu familia,”alisema Mbatia.
Taarifa ya Tume
Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”
Taarifa iliyotolewa Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk Mvungi alifariki dunia saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.
Iliendelea kusema taarifa hiyo kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini kuja nchini kwa maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu.
Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu sana, kwani ni mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo na dira yake.
“Tumepata pigo kubwa sana kwani tumempoteza mtu ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na aliyafahamu vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri aliyebobea katika constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi walimpenda sana,”alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi ambaye alikuwa naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu alipokwenda kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani kwake (kwa Mahalu).
“Wakati huo nilikuwa nikifundisha Ujerumani, alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na alifikia nyumbani kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa kazi, kweli tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.
Chadema, CCM wamlilia
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba taifa limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba Mpya.
“Tumepokea taarifa za kifo hiki kwa mshtuko mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Dk Mvungi, tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,” alisema Mbowe.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM), Mwigulu Nchemba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kutoa pole kwa Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya kazi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Alisema amekufa wakati mchango na mawazo yake yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali iwasake wahalifu hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho kimetokea wakati Dk Mvungi akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu na kwamba hali ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa kitaifa.“Tunahitaji kuangalia kiini cha uhalifu hapa nchini, watu wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni lazima tuchukue hatua,” alisema.
Mitandao ya kijamii
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii Forum ilikuwa ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.
Hussein Bashe kwenye ukurasa wake wa Facebook aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More (hatunaye tena), taarifa zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark, ndugu yetu Mvungi amefariki, mnamo saa tisa na nusu.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya jukumu zito kwa ajili ya taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu atalipia uhalifu huu, poleni Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni NCCR-Mageuzi.”
Mtu mwingine aliyechangia suala hilo kwenye mtandao wa Jamiiforum ni yule aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi aliyeandika kuwa, RIP Dr. Mvungi… Mungu akulaze mahala pema peponi. Japo umeondoka kivuli chako kitaishi… Naipa pole familia yako, maisha yetu kwa sasa nchini ni kudra za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe… wengine wamepona lakini wewe umeondoka.”

RIAS SHEIN AMEGEUKA MBOGO KWA WALE VIONGOZI WANAOTOA KAULI CHAFU JUU YA SERIKALI



muungano-shein_300_156
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein, amehadharisha juu ya kauli zinazotolewa na viongozi wa Serikali yake kuhusu masuala muhimu yanayoihusu Zanzibar. Amesema ni pamoja na msimamo wa visiwa hivyo kuhusu Katiba mpya, na kusema wanayoyatoa ni maoni yao binafsi na si msimamo wa Serikali.
Amesisitiza kuwa msimamo wowote wa Serikali, mwenye mamlaka ya kuusemea ni yeye na si mtu mwingine, kulingana na mamlaka ya kikatiba aliyopewa. Dk Shein alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari, baada ya kuelezea mafanikio ya Serikali ya SMZ awamu ya saba katika kipindi cha miaka mitatu tangu aingie madarakani.
“Naomba niliweke hili wazi, hakuna kiongozi yeyote awe waziri, makamu wa kwanza au wa pili wa Rais anayeweza kuisemea Zanzibar kuhusu jambo lolote isipokuwa mimi kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Katiba,” alisisitiza.
Moja ya maswali ya waandishi wa habari hao ni pamoja na kauli za viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni, akizungumza kuwa msimamo wa Zanzibar ni muundo wa Serikali ya Mkataba.
“Kama Makamu wa Kwanza wa Rais alizungumza kuhusu msimamo wetu wa Katiba, basi alikuwa akisema yake, au alikuwa akizungumzia chama chake, Katiba yetu iko wazi, kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake, hivyo kama ametoa msimamo kuhusu Katiba ni wake na si wa Serikali,” alisisitiza.
Dk Shein alisema anachojua yeye ni kwamba hadi sasa mchakato wa Katiba unaendelea vizuri na maoni ya Watanzania wakiwamo Wazanzibari ndiyo yatakayoamua muundo wa Serikali kwani hata yeye hana mamlaka ya kusemea Wazanzibari.
Aidha, Dk Shein alisema katika kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), unahitajika uvumilivu mkubwa na ushirikiano ili kuwa na nchi yenye amani na utulivu na inayotawalika.
Alisema jambo la msingi ambalo Serikali yake inalipa kipaumbele ni kuhakikisha kila kiongozi na mwananchi wa kawaida anafuata Katiba.
Kusaini mkataba Alitumia fursa hiyo kuvunja ukimya juu ya watu wanaomtuhumu kuwa alikwenda kinyume cha Katiba kusaini mkataba wa masuala ya utafiti wa mafuta akiwa Uholanzi na kutaka waliomzushia wafanye utafiti kwanza kabla ya kuropoka.
“Sijawahi kuvunja Katiba wala sitoivunja, nimefanya kazi serikalini tangu kipindi cha Rais Benjamin Mkapa na sasa Rais Jakaya Kikwete, naifahamu vema Katiba,” alisisitiza.
Alisema akiwa Uholanzi hakusaini Mkataba wa Nishati bali alisaini maelewano ya awali ya mkataba huo na kama kuna mtu ana ushahidi kuwa alisaini mkataba awasilishe ushahidi.
“Nimesikia haya kwenye vyombo vya habari tena cha kushangaza, wanaosema haya ni wanasheria, naomba wakilete hicho wanachokisema kuwa nimefanya, na maelewano ya aina hii si ya kwanza kusaini yapo niliyosaini mwaka 2011 mbona hawakusema?” Alihoji.
Pamoja na hayo, Rais pia alizungumzia masuala ya Muungano hasa eneo la mapato ambapo alisema masuala hayo mengi yako katika hatua ya mazungumzo, ili kufikia mwafaka kwa pande zote mbili.
“Si kweli kuwa tunasubiri Katiba kushughulikia masuala nyeti ya Muungano kama vile mgawanyo wa mapato, kwa sasa Zanzibar inapata asilimia 4.5 ya mgawo wa mapato kutoka Tanzania Bara, lakini kuna maeneo nyeti ambayo gharama za kuyaendesha nchi zote mbili zinagharimia, hivyo suala hilo linatafutiwa ufumbuzi kwa sasa,” alisema.
Mafanikio SMZ Katika kikao hicho, pia Dk Shein alizungumzia mafanikio ya Serikali yake kwa miaka mitatu tangu ishike uongozi kuwa ni makubwa katika maeneo mengi, ikiwamo kudumisha amani na utulivu visiwani.
“Hata hivyo, suala la watu kumwagiwa tindikali ndilo lililotia doa SMZ ndani na nje ya nchi hasa kitendo cha raia wa Uingereza kumwagiwa tindikali, kwa kweli nilisikitika sana na kiukweli Tanzania na hasa Zanzibar ilichafuka kwa vitendo hivi,” alisema.
Alifafanua, kwamba vitendo vya kumwagia watu tindikali vilianza mwaka 1995 na kukithiri miaka ya karibuni hadi sasa watu wanane wamekumbwa na mkasa huo, jambo ambalo Serikali imeanza kulifanyia kazi.
Alisema pamoja na changamoto iliyopo ya kutambua wahusika, Serikali zote mbili ya SMZ na Tanzania Bara, ziko katika mchakato wa kuangalia matumizi halisi na sababu za uingizwaji wa kemikali hizo nchini ili kuona namna ya udhibiti wake.
Kitovu cha uchumi Dk Shein alizungumzia pia mpango wa Serikali kuifanya Zanzibar kitovu cha uchumi Afrika Mashariki kwa kuhakikisha kuwa mji wa Unguja unajengwa upya kwa kufuata mipango miji ya kisasa.
Halikadhalika, alizungumzia namna Serikali yake imekuwa ikishughulikia masuala ya afya, elimu, utawala bora, utalii, viwanda na uchumi na kusisitiza kuwa sekta hizo sasa zimeboreshwa zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma kabla ya awamu ya saba ya Serikali yake.
“Niliingia madarakani mambo mengi yakiwa bado hayaridhishi, lakini kwa sasa mambo yanakwenda vizuri, kwani hata uchumi wakati nikiingia madarakani ulikuwa unakua kwa asilimia 6 .7 kwa sasa umepanda na kufikia asilimia 7.5,” alisema.